GREEN VOICES YATUA KINYEREZI NA KILIMO HAI.

GREEN VOICES YATUA KINYEREZI NA KILIMO HAI.

 

 Kikundi cha Green Voices Kinyerezi

 

Wanakikundi wakiwatika mbegu za mboga mboga kwa kutumia udongo maalum usio na kemikali.

 

Waandishi wa Habari wa Green Voices wakiwa na kiongozi wa kikundi cha Green Voices Kinyerezi Dr Sophia Mlote wa pili kushoto.

 

 

WAKATI dunia ikihaha kupambana na mabadiliko ya tabia nchi Wanawake  wa Kinyerezi Jijini Dar-e salaam wameamua kujikita katika KILIMO HAI kwa kuzalisha mbogamboga ambazo ni salama kwa maisha ya walaji wa bidhaa hizo.

Mtaalamu wa Kilimo Hai anasema, kilimo hicho kinatumia eno dogo, lakini pia unaweza kulima kwa mwaka mzima na kuacha udongo ukiwa salama   pasipo  kuharibu vyanzo vya maji.Mkurugenzi wa  T  -Organic Limited Bwana Abdul  Ally anasema kilimo hai kinafahamika duniani kwa kuzalisha mazao na mifugo pasipo kutumia kemikali.

Abdul anasema kilimo hai kinaweza kufanyika katika ngazi ya kaya, na kakihitaji mtaji mkubwa licha ya kuwa kinatumia mfumo wa malighafi  za kawaida yakiwamo majani, na mabaki ya chakula yasiyo na mchaganyiko wa kemikali.                                          

Bwana Abdul anasema hatma ya chakula salama itapatikana tu kwa kuzalisha mbolea iliyo salama kwani ndiyo inayoweza kuleta mafao  makubwa kwa kutumia mbolea za N’gombe, majani ,na dawa zinazopatikana kwenye chakula kama vile maziwa na maji ya Mchele na pilipili inayoweza kutumika kama  dawa  ya kufukuza wadudu katika mimea. Aidha anaongeza kuwa katika kuepuka madhara ya kemikali yanayopatikana katika chakula njia sahihi ni kulima kilimo hai kinachosaidia   kupambana  na magonjwa yanayoibuka huku waathirika wakubwa wa kemikali hizo ni kina mama kwani kemikali hizo zinasababisha magonjwa ukiwemo ugonjwa wa uvimbe wa wa tumbo la uzazi kwa wanawake.

 Naye Mtaalamu wa kilimo kutoka   Muungano wa wataalamu wa kilimo na wakulima  Tanzania (TAHA) Bwana Abdul Namalo amesema, ili kuondokana na tatizo la   kuzalisha chakula chenye sumu, ni lazima kubadili mfumo wa kilimo cha sasa   kwenda katika kilimo hai kwani kilimo hicho licha ya kuwa  rahisi pia kinaleta matokeo kwa muda mfupi   tofauti na kilimo kikubwa kinachotumia eneo kubwa la Ardhi pamoja na kuharibu  mazingira.

Dr. Sophia Mlote ni kiongozi wa mradi wa Green Voices kata ya Kinyerezi  anasema kilimo hai  ni maarifa mapya katika kilimo yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabia Nchi lakini pia yanaongeza kipato, na kuongeza lishe ya kaya “mazao yatokanayo na kilimo hai yana soko kubwa hivyo mazao yetu yatakuwa kwenye mnyororo wa thamani ambapo kutokana na ubora wa kilimo hai ni rahisi kupata soko ndani na Nje ya Nchi” anasema Dr Mlote.

Taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika kupitia mradi wa Green Voices ndio wadhamini wa mafunzo ya Kilimo Hai Kinyerezi ambapo mratibu   wa mradi huo Nchini Tanzania Bi Secelela Balisidya anasema, Taasisi hiyo   inalenga sana kuwakombea wanawake katika Bara la Afrika  na hasa ukizingatia kuwa wanawake ndio   wanaohusika na mazingira kupitia kazi zao za kila siku na hivyo kuunga mkono   juhudi zinazofanywa na wana sayansi katika kupambana na mabadiliko ya Tabia   Nchi hivyo mradi huo utasaidia kupaza sauti za wanawake katika Miradi kumi inayofanyika  hapa Nchini Tanzania na katika   kata ya Kinyerezi wanawake 15 wamenufaika na mradi huo.

Doreena Alphonce na   Christina Lwiza   ni wanufaika wa   mradi huo wanasema mafunzo waliyoyapata watayatumia kwa vitendo kwani   hawahitaji eneo kubwa kulima kwa mfumo huo ambapo  unaweza kulima kwa mfano wa bustani ya maua  au ndani ya nyumba na hata kwa kutumia gunia kwa kupanda miche 600 ya hoho au nyanya.

  Posted by: Tukuswiga Mwaisumbe at Thursuday, 12th MAY 2016