WANAWAKE WA BUKONGO WILAYANI UKEREWE WAMEITIKA WITO WA GREEN VOICES

 

Zao la muhogo ni chakula kikuu katika kisiwa cha kisiwa cha ukerewe ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa ukerewe mpaka kufika kipindi mkerewe akisema ana njaa ama hakuna chakula basi bila shaka ana maanisha kuna ukosefu au upungufu katika upatikanaji wa mihogo.

lakini kilimo cha mihogo siku za hivi karibuni kimekumbwa na changamoto kubwa kwani zao hilo limekuwa likishambuliwa na ugonjwa wa batobato ikiwa ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambapo kwa kiasi kikubwa wilayani hapo kimewaathiri wanawake ambao ndio uti wa mgongo wa kilimo kisiwani hapo kukiwa na idadi kubwa ya wanawake wafanyao shughuli za kilimo kulinganisha na wanaume.

Mbali na muhogo kuathiriwa na ugonjwa wa batobato na kuleta adha ya upatikanaji wa chakula ukerewe, kwa muda mrefu zao hili limekuwa likiwathiri wanawake wa ukerewe ambao kama wamama wa nyumbani walio na dhima ya uandazi wa chakula imekuwa ikiwawia vigumu katika shughuli za maandalizi ya chakula hiki hasa wakati wa kupika kwani ili chakula hiki kiive imekuwa ikiwagharimu kutumia kuni nyingi kuivisha na hivyo wakati mwingine wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kusaka kuni hizo hali wakikabiliana na mazingira hatarishi wakati wa zoezi hilo.

Lakini panapo ugonjwa bila shaka unahitaji tiba na vivyo hivyo kwa mabadiliko ya tabia nchi ambapo zinahitajika jitihada za maksudi kuyakabili mabadiliko haya na kupitia mradi wa sauti ya kijani ama green voices wanawake na wananchi wilayani ukerewe wamepata ahueni kwa kupata njia mbadala mbali na kilimo cha muhogo ambapo sasa wanawekeza nguvu zao katika kilimo cha viazi lishe ambavyo tofauti na mihogo zao hili si rahisi kukumbwa na ugonjwa wa batobato.

 

 

Posted by: Farida Hamis, on April 25th 2016.